Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Ijumaa, 6 Juni 2014

Kenya wanafunzi wanaenda na laptop shuleni Tanzania wanaenda na vidumu vya maji na fagio.

waziri mkuu Mizengo Pinda
Mbunge Maryam Salum Msabaha (Viti Maalum, Chadema), ameitaka serikali kutoa maelezo kuhusu chenji ya rada iliyotolewa ili kusaidia kupunguza tatizo la madawati katika shule za nchini kwa kuwa mpaka sasa wanafunzi wanaendelea kukaa sakafuni huku nchi jirani ya Kenya wanafunzi wake wakienda la Laptop.

Msabaha aliuliza katika kipindi cha maswali na majibu ya papo hapo ambayo hujibiwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kila Alhamisi.

Alisema nchi yoyote iliyoendelea duniani ilianza kuwekeza kwenye elimu na kutoa mfano wa nchi ya Malyasia, lakini hapa nchini watoto wanabeba madumu ya maji na fagio na kuketi sakafuni, wakati nchi jirani ya Kenya wanaenda na Laptop shuleni.

“Tuliambiwa chenji ya rada itapunguza tatizo mashuleni, lakini mpaka sasa watoto wanakaa chini na dawati moja wanakaa watoto mpaka watano,” alisema.

Akijibu, Waziri Mkuu  Pinda alisema jitihada ambazo serikali inafanya kuhusu elimu ni kuchukua maamuzi makubwa ambayo yamefanya suala la elimu kuzaa changamato kubwa kutokana na uandikishaji wa darasa la kwanza hadi la saba kuongezeka na kusababisha mahitaji  ya shule za sekondari, elimu ya juu ya vyuo vikuu kuongezeka.

Aliwataka Wabunge waendelee kusaidia serikali  ili bajeti ya Wizara ya Elimu iendelee kukua siku hadi siku kwani kukua kwa bajeti hiyo kutaongeza mambo mengi.

Katika swali  la nyongeza Msabaha alitaka kujua wakati huu wa utandawazi wa Sayansi na Teknolojia, serikali inachukua hatua gani kuona wanafunzi wa shule za msingi wanaanza kwenda shule na Laptop.

Hata hivyo, wakati akijibu, Waziri Mkuu Pinda alimhoji “unataka laptop kwa watoto wote wa shule inawezekana? Kwa sababu lazima uulize hilo swali.”

Alisema suala la wanafunzi wa darasa la kwanza mpaka la saba si kuwa na Laptop bali ni kuwa na mfumo wa digitali ambao utamwezesha vitabu vyake vyote kuwa ndani ya kompyuta kwa kutumia kifaa kinachoitwa tablets  badala ya kubeba mzigo mkubwa wa vitabu.