Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumatano, 9 Oktoba 2013

Mishahara ya viongozi tunaowachagua ni changamoto kupatikana kwa elimu ya bure nchini



HATIMAYE Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, ameweka wazi mshahara wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Zitto ameutaja mshahara huo wa Pinda anayejitambulisha kama ‘mtoto wa mkulima’ juzi mjini Mpanda na jana wilayani Sikonge wakati akihutubia mikutano ya hadhara katika ziara ya Kanda ya Magharibi kwa ajili ya ujenzi wa chama.

Alisema Pinda anapokea jumla ya sh milioni 26, ambazo ni kiasi kikubwa kulinganisha na uchumi wa nchi.

Akichanganua alisema Pinda anapokea sh mil. 11.2 kama mbunge, sh mil. 8 kwa nafasi ya waziri na kiasi kinachosalia kufikia sh mil. 26 kwa nafasi yake ya uwaziri mkuu.

Alisema sababu hiyo ya mishahara mikubwa isiyokatwa kodi ndiyo huwafanya viongozi wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa wakali pale vyombo vya habari vinapotaka kuwafahamisha wananchi namna watumishi wao wanavyojilipa.

“Nimeanza na mshahara wa waziri mkuu pia siku zijazo nitataja na wa rais, kwa kuwa amesaini makubaliano na Serikali ya Marekani kuendesha nchi kwa uwazi, na moja ya uwazi ni kwa muajiri kujua kiasi anachomlipa mwajiriwa wake,” alisema Zitto.

Hatua ya Zitto imekuja baada ya kuwapo mvutano mkubwa kuhusiana na kile kinachodaiwa ‘usiri’ wa mishahara ya watumishi wa umma, wakati ni haki ya walipa kodi kujua kile wanachowalipa walioomba kuwaongoza.

Kodi ya laini za simu

Akizungumzia sakata la kodi katika laini za simu, Zitto alisema CCM ina ajenda ya kisiasa kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2015.

Alisema serikali baada ya kubaini watu wengi wanapeana taarifa kwa njia ya ujumbe mfupi, hususan katika masuala ya kisiasa, wakaona njia sahihi ya kudhibiti ni kuwatoza kodi ya laini ili kupunguza hatari ya mawasiliano hayo kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao.

“Sikuwepo bungeni wakati wabunge wa CCM wanapitisha kadhia hiyo ya kuwanyonya wananchi, wenzangu wakaniambai tukasema hapana, kwa maana tuliona hii leo kuna Watanzania wengi wasio na uwezo wa kuhudumia simu kwa kiasi cha sh 1,000 kwa mwezi,” alisema Zitto.

Akijibu maswali ya wananchi mjini Mpanda waliotaka kujua sababu ya kupunguza makali bungeni, Zitto alisema hakuna makali yaliyopungua bali ni mitazamo ya watu.

Alisema kwa kushirikiana na wabunge wenzake wa upinzani wamekuwa wakisimamia hoja zenye manufaa kwa wananachi huku wabunge wanaojipambanua kuwa majasiri kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiwaunga mkono wazi wazi.

Akiwa wilayani Sikonge, Zitto alisema Watanzania hawawezi kujivunia uhuru huku mama zao, watoto wao na wazee wao wakiwa hawana uhakika wa kupata huduma bora ya afya, elimu na maji safi.

Alisema kwa sasa Tanzania ni taifa moja lililogawanyika katika nchi mbili za wenye fedha na wasio na fedha.

Alisema nchi ya wenye fedha, familia zao husoma katika shule bora, zenye mazingira bora na walimu wazuri, hutibiwa katika hospitali zenye hadhi na huduma muhimu na ikibidi nje ya nchi, huku nchi ya wasio na fedha familia zao wakiishi kwa shida, kusoma katika majengo ya shule na walimu wasiopata mishahara ya kuridhisha na hospitali zisizokuwa na huduma muhimu licha ya kuchangia kiasi cha fedha kwa ajili ya bima ya afya.

(chanzo Tanzania daima)

wanafunzi kidato cha pili wafanya mtihani

Dar es Salaam. Jumla ya watahiniwa 531,457 wa kidato cha pili wanatarajia kufanya mtihani utakaoanza kesho Oktoba 7 hadi 21 mwaka huu.Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome  alisema mitihani hiyo itafanyika kwa wiki mbili.
Alisema kati ya idadi hiyo, wasichana ni 270,734  sawa na asilimia 50.9 na wavulana ni 260,723 sawa na asilimia 49.1.Mchome alisema katika taarifa yake kwamba idadi ya shule na vituo vilivyosajiliwa kufanyia mtihani huo mwaka huu ni 4,437  ikiwa ni ongezeko la vituo 140 sawa na asilimia 3.3 ikilinganishwa na vituo 4,297 vilivyosajiliwa mwaka 2012.
Alisema watahiniwa waliojiandikisha wanajumuisha makundi maalum yenye uoni hafifu, ambao ni 89 na wasioona 93.ìKaratasi za mtihani wa watahiniwa wenye mahitaji maalum zimeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji yao kama vile kutumia karatasi za maandishi yenye nundu kwa wasioona na kuongeza ukubwa wa maandishi kwa wenye uoni hafifu,î alisema.
Mchome alisema umuhimu wa mtihani huo ni kupima kiwango cha maarifa na ujuzi alioupata mwanafunzi kutokana na mada alizojifunza katika kidato cha kwanza na cha pili.
Pia alisema mtihani huo unatoa changamoto zinazosaidia wanafunzi, walimu, wizara na wadau wa elimu kutambua mapungufu yaliyopo katika ufundishaji ili yaweze kufanyiwa marekebisho kwa lengo la kuboresha elimu.
chanzo. mwananchi.co.tz

Wanafunzi 2,446 hawapati chakula cha WFP






IMEELEZWA kuwa wanafunzi 2,446 waliopo katika shule za msingi za wilayani Bahi, mkoani Dodoma, hawapati chakula kinachotolewa kwa msaada na Shirika la Chakula Duniani (WFP) kutokana na shule hizo kukosa majengo ya kuhifadhi chakula.

Hayo yalibainishwa jana na Ofisa Elimu wa Shule za Msingi Bahi, Mary Mathew.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Mary alisema ukosefu wa majengo unatokana na wazazi kutokuwa tayari kujitolea kujenga.

Alisema msimamo wa WFP uko wazi kwamba hawako tayari kutoa chakula kwenye shule zisizo na majengo ya kuhifadhiwa chakula.

Alieleza kuwa katika Wilaya ya Bahi, kuna shule za msingi 72 na kati ya hizo shule saba hazipati chakula cha mchana kutokana na wazazi kutoitikia mwito wa kujitolea.

Ofisa Elimu huyo alisema hali ya kukosekana kwa huduma ya chakula kwenye shule hizo imesababisha utoro kwa wanafunzi.

Shule ambazo hazipati chakula cha mchana ni pamoja na Nholi, Bakolo, Chikopelo Nhinyila, Tinai, Mgondo na Bahi Misheni.
 
Chanzo. Marafiki wa elimu dodoma