Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Alhamisi, 19 Septemba 2013

wasichana 11 shule ya msingi wapata mimba

WASICHANA 11 wa shule ya msingi iliyo Ndhiwa, Kaunti ya Homa Bay, wamepatikana kuwa wajawazito. Wanafunzi hao wa Shule ya Msingi ya Rangenya, iliyo karibu na Ndhiwa mjini wanajumuisha msichana mwenye miaka kumi aliye katika darasa la saba. Wawili kati yao tayari wananyonyesha watoto baada ya kujifungua hivi majuzi.

Wasichana wawili wako katika darasa la saba, huku kukiwa na mmoja katika darasa la nne na mwingine darasa la tano.Duru za kuaminika zilisema waliohusika kuwapachika watoto hao mimba ni mwalimu aliyeajiriwa na Chama cha Walimu na Wazazi (PTA), waendeshaji boda boda na vijana wanaotoka katika vijiji vya karibu.

Mwalimu huyo ambaye ni jamaa ya mmoja wa walimu wenye vyeo vikuu shuleni humo alipelekwa hadi kituo cha polisi mwaka jana, kwa kudaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mmoja wa wanafunzi aliye katika darasa la saba.

Shughuli katika shule hiyo zilisitishwa kwa muda Jumanne baada ya Mkuu wa Elimu katika wilaya hiyo Maurice Jayora, na maafisa wake walipowasili kuanzisha uchunguzi.
Maafisa hao walitumia saa kadha asubuhi kuhoji walimu na wanafunzi kuhusu tukio hilo.

Mkuu huyo wa elimu aligutushwa na hali kuwa wasimamizi wa shule hiyo hawajawahi kufahamisha afisi yake wala ile ya afisa wa elimu katika eneo hilo kuhusu matukio hayo.“Nataka ifahamike kuwa mimi na maafisa wangu, tulifahamu kuhusu tukio hili kupitia vyombo vya habari. Hata afisa wa elimu katika eneo hili hakujulishwa,” alisema.

Masomo

Alithibitisha kuwa baadhi ya wasichana walioathirika bado wanaendelea na masomo na wanasaidia kwenye uchunguzi.“Baadhi ya waathiriwa ambao bado wako shuleni wanatupatia habari muhimu zitakazosaidia kwenye uchunguzi tunaofanya,” alisema.

Juhudi za kukabiliana na matukio kama haya pamoja na kuozwa kwa wasichana wenye umri mdogo katika maeneo ya Ndhiwa na Homa Bay hazijafua dafu kutokana na ukosefu wa ushirikiano kutoka kwa wazazi. Uchunguzi umebainisha kuwa wakati wowote wanaohusika wanapokamatwa, baadhi ya wazazi huingilia kati na kupendelea kutohusisha mahakama kutatua masuala hayo.

Naibu wa Kamishna wa Kaunti Geoffrey Omonding amekuwa akionya maafisa wa utawala kuhusu athari iliyopo ikiwa matukio kama haya yatapatikana kuwa yanatokea katika maeneo wanayosimamia.