Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumanne, 17 Septemba 2013

CHAMA CHA HISABATI TANZANIA CHAPINGA (multiple choice) MITIHANI YA TAIFA YA HISABATI

CHAMA cha Hisabati Tanzania (MAT) kimeitaka Serikali kuliagiza Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), kuondoa mfumo wa majibu ya kuchagua (multiple choice) kwenye Mitihani ya Taifa ya Hisabati kwa shule za msingi nchini. MAT imesema mfumo huo unapunguza uwezo wa kufikiri na kutafuta majibu sahihi kwa wanafunzi na kusababisha taifa kupoteza vipaji vya somo hilo na kushusha viwango vya ufaulu nchini.
Mwenyekiti wa MAT, Dk. Sylvester Rugeihyamu alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa mwaka wa chama hicho jijini Mbeya.Dk. Rugeihyamu alisema mfumo huo hauna athari za kufikiri kwa mantiki kwa wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo vikuu lakini unapunguza uwezo wa kufikiri kwa wanafunzi wa shule za msingi kwa sababu bado wanahitaji mazoezi mengi ya kukuza uwezo wao wa akili.
Alisema mfumo huo unawafanya wanafunzi kubahatisha majibu badala ya kutumia uwezo wao wa akili hali inayodumaza vizazi vya Tanzania katika kumudu masomo yanayohitaji umakini wa fikra.
“Inawezekana huu mfumo ulianzishwa kwa lengo la kubana matumizi, lakini utadumaza watoto na taifa zima litarudi nyuma katika elimu, kwa kweli huu mfumo siyo mzuri kwa watoto wadogo,” alisema.
Dk. Rugeihyamu aliitaka NECTA na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuchukua hatua za kuacha matumizi ya mfumo huo kuliokoa taifa na hatari ya kuwa na vijana wasiokuwa na uwezo mzuri katika taaluma.
Dk. Rugeihyamu alisema mfumo huo pia umechangia kushuka kiwango cha ufaulu kwa somo la hisabati nchini tangu ulipoanza kutumika mwaka 2011 ambako kiwango cha ufaulu kilikuwa ni asilimia 39.36 lakini kikashuka hadi asilimia 18.74 mwaka 2012.
mtanzania.co.tz