Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumanne, 29 Julai 2014

ZAIDI YA WANAFUNZI 860 WA SEKONDARI WILAYANI KILINDI WAMEACHA SHULE.


Wanafunzi zaidi ya 860 wa shule mbali mbali za sekondari wilayani Kilindi wameacha shule kwa sababu mbali mbali ikiwa ni pamoja na baadhi ya wazazi wao kuwaozesha huku wengine wakiwekwa kinyumba na baadhi ya makundi ya vijana.
Mkuu wa wilaya ya Kilindi bwana Selemani Liwowa amesema hayo katika kikao cha baraza la madiwani ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mheshimiwa Dr . Jakaya Kikwete kuwataka viongozi wa mkoa wa Tanga kuhakikisha kuwa watuhumiwa waliosababisha tatizo hilo wanakamatwa na kufunguliwa kesi katika vyombo vya sharia.
Akielezea mikakati waliyojiwekea na hatua zitakazochukuliwa mkuu huyo wa wilaya amesema kwanza wanataka wawarejeshe watoto hao kwa wazazi kisha watawakamata wazazi na watuhumiwa waliowakatisha masomo kwa ajili ya kuwachukulia hatua kali za kisheria zoezi ambalo linaanza utekelezaji wake baada ya sikukuu ya eid kumalizika.


chanzo ITV

Wanafunzi 140 wakwepa masomo tunduma na kujihusisha na biashsra ndogondogo.

Zaidi ya wanafunzi 140 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu katika halmashauri ya mamlaka ya mji mdogo wa Tunduma wilayani momba mkoani Mbeya bado hawajaripoti shuleni kuanza masomo na badala yake wanadaiwa kujihusisha na biashara ndogondogo kama vile kuuza karanga na kubeba mizigo mpakani mwa Tanzania na Zambia mjini Tunduma.
Akizungumza kwenye baraza la halmashauri ya mamlaka ya mji mdogo wa Tunduma, mwakilishi wa mkuu wa wilaya ya momba ambaye pia ni katibu tawala wa wilaya hiyo, Mathias Mizengo amesema kuwa halmashauri ya mamlaka ya mji mdogo wa Tunduma inakabiliwa na changamoto ya baadhi ya vijana ambao wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu kutoripoti shuleni na hivyo akawataka viongozi wa mamlaka hiyo kuhakikisha vinaja hao wanatafutwa kila mahali walipo na kuwapeleka shuleni.
 
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Juma Kitabuje amesema kuwa hadi kufikia mwezi juni mwaka huu wanafunzi 144 kati ya wanafunzi 956 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika mji wa Tunduma ndio ambao walikuwa hawajaripoti shuleni kati yao wanafunzi 70 wakiwa ni wavulana na wanafunzi 74 wasichana huku akielezea sababu kubwa ya watoto hao kutohudhuria masomo kuwa ni kutelekezwa na wazazi na kujihusisha na biashara za kuuza karanga na kubeba mizigo mpakani.
 
Kuhusu hatua ambazo zinachukuliwa na mamlaka hiyo kuhakikisha kuwa wanafunzi hao wanaendelea na masomo, mkurugenzi huyo amesema kuwa wazazi wa watoto hao wamefikishwa kwenye baraza la kata na kupewa muda hadi kufikia Agosti 25 mwaka huu kuwasaka watoto wao popote walipo na kuwapeleka shuleni.

Kwa wasiomfahamu mwalimu.

Mwalimu JK Nyerere

1. Ndiye rais aliyewahi kulipwa mshahara kidogo duniani
 
2.ndiye mtu aliyeitetea china isitengwe na UN, baada ya mataifa yote kuogopa vtisho vya marekani, wachina wanamtambua na kumheshimu sana

 
3. Ndiye rais pekee aliyetishia kuvunja balozi za uingereza, ujeruman na ufaransa na hata kukataa msaada wao kwa kitendo chao cha kuunga mkono serikali ya kibaguz afrika kusini

 
4. Ndiye rais aliyewezesha watoto wa masikin wasome bila ada na matibabu bure. Nenda nchi za kenya, afrika kusini . Kama baba yako hakushirik harakati za ukomboz ili utoke labda uwe jambaz maana huwez hata kujilipia ada


Ndiye rais pekee aliyechukia ufisadi toka moyoni.

Jumanne, 22 Julai 2014

binti aliyekeketwa alilia shule

 Akiwa darasa la nne alikamatwa kwa nguvu..
Mama mzazi wa binti muathirika wa ukeketaji akifafanua 
Mama mzazi wa binti muathirika wa ukeketaji akifafanua jambo huku akisikilizwa na binti yake.
Kuna mambo mengi anakumbukia msichana mwenye umri wa miaka 12  yamemtokea maishani. Lakini tukio la siku hiyo, kuitwa na mama yake mdogo, kisha kukamatwa kwa nguvu na kukeketwa  linabaki kuwa kovu lisilopona katika maisha yake. Ni ukatili uliopitiliza uliobadili kabisa ndoto za maisha yake za kupata elimu.
 
Binti wa miaka 12 (jina linahifadhiwa)  ni mtoto wa mwisho wa kike kati ya watoto nane wa mzee Isaya na Mama Gyar Baa kutoka familia moja ya kabila la Kimbulu.
 
Kabla  hajakumbwa na mkasa uliobadilisha kabisa welekeo wa maisha yake, alikuwa mwanafunzi wa darasa la nne mwenye  ndoto za kusoma hadi kufikia ukomo wa maisha yake.
Hata hivyo, ndoto hizo zilizimwa baada ya  kujikuta akilazimishwa kukeketwa ikiwa ni ishara ya maandalizi ya kutafutiwa mume ili aolewe.Tukio hilo la kikatili liliathiri maisha yake.
 
Makazi ya familia ya binti huyo ni katika kijiji cha Konje wilaya ya Handeni mkoani Tanga, kilichopo umbali wa kilometa 16 kutoka Handeni mjini.
 
Msichana huyo, anatoka katika familia ya wafugaji, yenye tabia ya kuhamahama ili kufuata malisho, hasa nyakati za ukame ili kuhakikisha kuwa mifugo yao haikosi chakula na maji.

Akisimulia kwa uchungu mkasa alioupata uliobadili kabisa uwelekeo wa maisha yake, msichana huyo anasema siku hiyo ya Jumanne (hakumbuki tarehe) aliitwa na mama yake mdogo (mama wa kambo). Aliitika na kutii amri kwa kwenda kusikiliza alichoitiwa akiwa hana fununu kabisa ya dhamira ya muitaji.
 
Anasema baada ya kufika nyumbani kwa mama yake huyo, alishangazwa kumkuta dada yake anayemfuata (jina linahifadhiwa) akiwa amefungwa mikono na miguu huku akilia kwa uchungu sana. Kilichomsikitisha zaidi ni kuona jinsi ambavyo dada yake alikuwa akivuja damu nyingi katika sehemu zake za siri.
 
Jambo hilo, lilimtisha sana Tansiana na kutokana na hamaki akapata wazo na maamuzi ya haraka ya kukimbia  kutoka nyumbani kwa mama yake mdogo  ili kujinusuru na hatari aliyoona kuwa inamkabili. Hata hivyo, hakufanikiwa kutimiza matakwa yake.
 
“Nilishtuka sana, kumuona dada akilia huku damu zinamtoka kwa wingi  sana katika sehemu zake za siri. Lakini nilivyotaka kukimbia mama mdogo  na bibi yule niliyemkuta pale nyumbani ambaye sikufahamu ametokea wapi wakanikamata na  kunifunga mikono na miguu kwa kamba,” anasimulia msichana huyo kwa masikitiko.
 
Baada ya kufungwa na kudhibitiwa kikamilifu ndipo bibi huyo asiyemfahamu akachukua kiwembe na kumkata kwenye sehemu yake ya siri kwa namna alivyojiridhisha na kusababisha atokwe damu nyingi kama ilivyokuwa kwa dada yake.
 
“Wakati  wananikata sikusikia maumivu sana kwa sababu nilikuwa na hasira sana kwa kile kitendo nilichokiona amefanyiwa dada yangu…ndipo  baada ya kupita muda kama kama saa moja hivi nikaanza kusikia maumivu makali sana kama roho inataka kutoka. Ndipo nikatambua namna gani watu wale walivyo wakali. Nilikuwa nimefanyiwa unyama wa hali ya juu bila ya ridhaa yangu. Nililia sana na kwa hakika nimemchukia sana huyo mama mdogo na sijui kama nitamsamehe,” anasema.
 
Akikumbukia zaidi anasema kuwa “wakati wananifanyia unyama huo, mama yangu mzazi alikuwa amesafiri kwenda Karatu na baba  hakuwapo nyumbani. Aliporudi alikuta tayari tumekeketwa.”
 
Anabainisha kwamba, ilimchukua takriban mwezi mmoja kuuguza kidonda hicho hadi kupona. Aina ya matibabu aliyokuwa akipewa anasema kuwa, ni kupakwa maziwa na mafuta ya taa mara mbili kwa siku.Yaani asubuhi na jioni kama dawa ya kuponyesha jeraha hilo. Alipata msongo mkali wa mawazo kuhusu tukio hilo baya kabisa na la ukatili wa kupindukia.
Baba yake, licha ya kutabua unyama waliofanyiwa, lakini hakuchukua hatua zozote dhidi ya wahalifu wale.
 
Anasema kuwa, miongoni mwa sababu walizoelezwa zilizolazimisha wachukuliwe hatua hiyo kukeketwa ni watoto wa kike kuwafanya waachane na vitendo vya uhuni kwa kile kinachodaiwa kuwa, wasipokeketwa wanakuwa na tamaa kali ya  kufanya mapenzi muda wote.
 
Hii ni kutokana na mila na desturi za kabila lao, kwamba iwapo binti hatakeketwa, basi ni dhahiri kwamba hatapata mume wa kumuoa na hatakuwa na heshima wala thamani anayostahili kupewa mwanamke kwenye jamii hiyo.
 
Kutokana na kitendo hicho, anasema kuwa ni dhahiri kwamba ameandaliwa kwa ajili ya kuolewa, hata kama jambo hilo litafanyika litakuwa ni kinyume cha ridhaa yake.
 
“Najua sasa hivi nasubiri tu kuolewa. Lakini ni kwamba watanilazimisha tu lakini mimi mwenyewe sipendi…napenda sana kusoma… natamani sana ajitokeze mtu wa kunisaidia katika hilo. Nipo tayari kabisa kwa hilo…na baada ya kusoma cha kwanza nitakachofanya ni kuhakikisha nazuia mila hii mbaya isiendelee kufanyika kwa wasichana wengine wa jamii hii. Kwa kweli inauma sana…tunateseka sana jamani,” anasema msichana huyo huku akibubujikwa machozi.
 
Msishana huyo, licha ya hatua ngumu ya maisha yake aliyopitia, lakini ana matumaini kuwa, siku moja atakuwa mwanaharakati wa kutetea haki za wanawake, na kupiga vita mila na desturi ambazo zimekuwa zikitumika kumgandamiza mwanamke.
 
Aina hiyo ya maisha, ndiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kumfanya msichana huyo kuwa miongoni mwa wale waliokosa fursa ya kupata haki yake ya msingi hasa elimu. Alikuwa na ndoto za siku moja kupata elimu ili uwe mwanga wa uhakika kwa maisha yake na jamii yake inayomzunguka.
 
Pamoja na kukabiliwa na changamoto hiyo maishani, lakini binti huyo  katika familia yake ana msimamo wa kupenda elimu na kujituma kwa kazi za kifamilia na kwamba iwapo atatokea mfadhili yoyote atakayekuwa tayari kumchukua na kwenda kumsomesha  hata wazazi wake sasa wameutambua ukweli huo na kuwa tayari kumruhusu aende akapate elimu.
 
“Kamwe sitasahau unyama huu…nikipata elimu lazima niwe mwanaharakati wa kupinga unyama huu ,” anasema.
Mama mzazi wa binti huyo aitwaye Gyar Baa Isaya anasema kuwa wakati binti yake anakeketwa, alikuwa safarini na hakushirikishwa na mumewe kuhusu kufanyika kwa kitendo hicho.

Kimsingi anasema, alikuwa anafahamu kuwa siku moja binti yake atalazimika kufanyiwa mila hiyo kwa sababu ni utamaduni ambao hata yeye ameupitia na hakuwa na mamlaka ya kuupinga, kwani kwa kufanya hivyo, angeweza kumsababishia matatizo mtoto wake ikiwamo kutoolewa.

“Kusema kweli kwa mila za kwetu ili uonekane ni mwanamke ambaye umekamilika ni lazima ukeketwe…vinginevyo hupati mume na unaweza kupatwa na majanga makubwa  ikiwamo binti kuanza tabia mbaya kabla ya wakati wake…sasa watoto wangu wamelazimika kufanyiwa mila hiyo ingawa hawakuridhika nayo kabisa,” anasema mama huyo.

Naye  dada wa msichana huyo aliyeanza kufanyiwa ukatili huo, anasema kuwa sababu kubwa ya mdogo wake kushindwa kuendelea na masomo licha ya kuwa na ndoto za kufika mbali kimaisha ni ile hofu ya kuchekwa na wenzake hasa wakati wa kuoga wakimuona amekeketwa.

“Unajua mnapokuwa rika moja mnakuwa hamuoneani aibu kabisa, hata kama kuoga mtaenda wote, sasa wenzako wakikuona uko tofauti na wao kimaumbile wanakushangaa na wengine wanakucheka. Hali hii nilipokuwa nikimwelezea mdogo wangu ilichangia kumkatisha tamaa ya kusoma kwa hofu ya kuchekwa,” anasema dada huyo ambaye  ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule moja.

Hata hivyo anasema, kitendo walichofanyiwa kinadhihirisha udhalilishaji kwa mtoto wa kike na kwamba licha ya baba yao kuwa ni miongoni mwa wafugaji wenye tabia ya kuhamahama, lakini amedhamiria kuhakikisha kuwa anamaliza masomo yake.

“Baba yetu ni miongoni mwa wafugaji wenye tabia ya kuhamahama makazi, hali hii imetuathiri sana kielimu tena mimi ni nafuu kwa sababu naishi kwenye hosteli za shule. Mdogo wangu ndiyo amerudi nyuma kwani hadi sasa hasomi na  aliishia darasa la nne,” anasema dada huyo.
CHANZO: Ippmedia.com

Jumamosi, 19 Julai 2014

Waliohitimu la 7 Vijibweni waitwa kuchukua vyeti



BAADA ya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Vijibweni, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, Mathew Jasembe kutuhumiwa kupoteza vyeti vya wanafunzi 247 waliohitimu darasa la saba mwaka 2011 amewataka wafike shuleni kuchukua vyeti vyao.
Tuhuma hizo ziliibuliwa na baadhi ya wazazi wa wanafunzi hao, wakisema wamechoshwa na ahadi za mwalimu huyo kwa zaidi ya miaka miwili sasa tangu vyeti hivyo kupotea, ziliandikwa na gazeti hili hivi karibuni.
Wazazi hao walidai mkuu huyo alihusika kwa sababu hakuwa wazi kueleza mazingira halisi ya jinsi vyeti hivyo vilivyopotea na kwamba hakupenda suala hilo lifike ngazi za juu.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, mwalimu huyo, alisema tofauti zilizojitokeza awali hadi kusababisha vyeti hivyo kuchelewa kukabidhiwa kwa wahitimu zimepatiwa ufumbuzi na vyeti hivyo vipo tayari.
Alisema baada ya mchakato wa kuviandaa vyeti hivyo kukamilika tangu juzi, klichobaki ni kuwakabidhi wahitimu hao.
“Mbona nimeanza kuwakabidhi wachache waliopata taarifa… nimeweka matangazo katika eneo linalozunguka shule kwa ajili ya kuwajulisha kuwa vyeti vyao vipo tayari ni wao wenyewe sasa.
“Niwaombe wazazi kupitia gazeti lenu wa waambie watoto wao waende shuleni hapo wakachukue vyeti vyao,” alisema Jasembe.
Hivi karibuni wazazi wa watoto hao, walifikisha tuhuma hizo kwa Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndugulile, Ofisa Elimu na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke.

Jumatano, 16 Julai 2014

SHULE YA ISANGO ILIYOKUWA IKIMILIKIWA NA JUMUIYA YA WAZAZI CCM YAUZWA KWA BEI CHEE

Photo: shule ya sekondari Isango iliyoko Kinesi Wilaya ya Rorya mkoa wa Mara imeuzwa kwa bei sawa na bure ya sh. milioni 125

wakizungumza kwa nyakati tofauti mwenyekiti wa ccm na mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi wilaya ya Rorya kupitia kituo cha radio Victoria Vfm wamedai kuwa shule hiyo imeuzwa kijanja janja kwani tangu mwenyekiti huyo wa wazazi aingie madarakati hakuwahi kuambiwa juu ya uwepo wa deni lililopelekea kuuzwa shule hiyo.
mwenyekiti huyo wa jumuiya ya wazazi alienda mbali zaidi na kusema kitendo hicho kimefanywa makusudi kwa lengo la kumharibia uwajibikaji wake kwani kadai aliyeinunua shule hiyo ni mtoto wa aliyekuwa Mwenyekiti wa wazazi ccm mkoa wa Mara.
pia kasema kuwa dalali alionyesha wazi muenendo wa rushwa, kwa kugonga nyundo ya mwisho wakati bado wateja wengine wakiendelea kupandisha dau.

baada ya hapo ametoa wito kwa wananchi kumuunga mkono ili kuhakikisha shule hiyo inarejeshwa kwa wananchi baada ya kuwaambia wananchi hao kuwa tayari wamekwisha fungua kesi mahakama ya rufaa na hivi karibuni atakwenda kuonana na katibu mkuu wa chama cha mapinduzi ili kuhakikisha shule hiyo inarejeshwa mikononi mwa wananchi.shule ya sekondari Isango iliyoko Kinesi Wilaya ya Rorya mkoa wa Mara imeuzwa kwa bei sawa na bure ya sh. milioni 125

wakizungumza kwa nyakati tofauti mwenyekiti wa ccm na mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi wilaya ya Rorya kupitia kituo cha radio Victoria Vfm wamedai kuwa shule hiyo imeuzwa kijanja janja kwani tangu mwenyekiti huyo wa wazazi aingie madarakati hakuwahi kuambiwa juu ya uwepo wa deni lililopelekea kuuzwa shule hiyo.
mwenyekiti huyo wa jumuiya ya wazazi alienda mbali zaidi na kusema kitendo hicho kimefanywa makusudi kwa lengo la kumharibia uwajibikaji wake kwani kadai aliyeinunua shule hiyo ni mtoto wa aliyekuwa Mwenyekiti wa wazazi ccm mkoa wa Mara.
pia kasema kuwa dalali alionyesha wazi muenendo wa rushwa, kwa kugonga nyundo ya mwisho wakati bado wateja wengine wakiendelea kupandisha dau.

baada ya hapo ametoa wito kwa wananchi kumuunga mkono ili kuhakikisha shule hiyo inarejeshwa kwa wananchi baada ya kuwaambia wananchi hao kuwa tayari wamekwisha fungua kesi mahakama ya rufaa na hivi karibuni atakwenda kuonana na katibu mkuu wa chama cha mapinduzi ili kuhakikisha shule hiyo inarejeshwa mikononi mwa wananchi.

Jumatano, 9 Julai 2014

Tunataka wapate maarifa au wajue Kiingereza? makala ya Gervas Zombwe.

Tafiti zote duniani zinasema wazi kuwa binadamu yeyote anajifunza na kuelewa kikamilifu anapofundishwa kwa lugha anayoijua zaidi. Na uwezo wa kujenga utambuzi na kukuza vipawa umo ndani ya mila na desturi asilia zinazofungamana moja kwa moja na lugha mama inayomiliki maarifa na michepuo ya akili.
Kufundishwa kwa lugha asiyoielewa vizuri kunamzuia binadamu kumiliki maarifa ya kukuza michepuo ya akili. Kweli atasoma, atapata cheti, digrii, lakini maarifa na ubunifu viitabaki nje ya utambuzi wake.
Ndiyo maana nchi zote zilizoendelea wanafundisha watu wao kwa lugha zao. Huwezi kubuni kwa kutumia lugha ya jirani, huwezi kufikiri kwa kutumia lugha ya kukopa, kuwezi kuvumbua kwa kutumia lugha ya kigeni. Ni ndoto!
Mwalimu wa lugha, mtafiti na mtetezi wa lugha Profesa Martha Qorro, siku zote kupitia tafiti nyingi alizofanya amekuwa akisisitiza manufaa ya kutumia lugha ya taifa kufundishia vijana wetu.
Ili mwanafunzi afike ngazi ya juu kabisa ya uelewa, ni lazima maarifa yapitie kwenye lugha anayoijua vizuri. Vinginevyo atakuwa anajifunza juu juu tu na kuishia kwenye uelewa wa hatua ya mwanzo tu. Hatua za uelewa ziko kama ifuatavyo:
Hatua ya kwanza, uwezo wa lugha ya ‘kuombea maji’. Akilazimika kujifunzia lugha katika ngazi hii mzungumzaji inabidi akariri karibu kila kitu kwa kuwa ana uelewa mdogo. Huchukua muda mrefu kuelewa mambo madogo kwa kuwa lugha ni kikwazo. Haoni uhusiano kati ya maisha yake na mambo yale anayofundishwa au anayoelezwa shuleni. Masomo humchosha na mawazo huhama darasani.
Hatua ya pili, uwezo wa kumpa mtu maelekezo ya namna ya kufika sehemu fulani. Uelewa wa juu juu wa mambo yanayozungumzwa au kufundishwa kwa lugha hiyo. Tabia ya kukariri bado inaendelea, ingawa imepungua kwa kiasi kikubwa. Uwezo wa kuandika sentensi fupi fupi sahihi na kuuliza maswali rahisi. Kuna uwezekano mkubwa wa kutoelewa au kuelewa vibaya maana iliyokusudiwa. Uhuru wa fikra haupo!
Hatua ya tatu, uwezo wa kufikiri, kutafakari, kujadili, kuchambua na kuchanganua masuala na dhana mbalimbali yanayozungumzwa au kufundishwa kwa lugha husika. Mzungumzaji anakuwa na uwezo mkubwa wa kutumia lugha kama nyenzo ya kuvumbua mambo mapya. Ana uhuru wa kutumia lugha husika na yote atakayoelezwa katika kujikomboa kimawazo.
Katika hatua hii, lugha siyo kikwazo katika kuelewa, kupambana na changamoto za maisha. Hahitaji kukariri; bali hutumia uelewa wake katika kujibu maswali au kutoa maelezo juu ya yale anayoyaelewa. Ni katika hatua hii ya uelewa ndiyo wanafunzi wanapoweza kujifahamu, kujitambua, kuwa mbunifu, kutumia fursa, kujiendeleza, kutafiti na kutatua changamoto zinazomzunguka. Wanafunzi wetu wengi shuleni na vyuoni hawafiki hatua hii. Ushahidi unaonyesha shule za sekondari hawajifunzi na kupata maarifa kutokana na lugha. Kwa mfano, tafiti nyingi (Mlama na Matteru 1978, Criper and Dodd 1984, Roy-Campbell and Qorro 1987, Rubagumya, Jones and Mwansoko 1998, Qorro 1999, Mwinsheikhe 2003, Puja 2003, Brock Utne 2004, Vuzo 2005) zimeonyesha kuwa wanafunzi wengi katika shule za sekondari na vyuo nchini Tanzania wana uwezo wa hatua ya kwanza au ya pili ya uelewa wa lugha inayotumika kufundishia.
Kwa kung’ang’ania kutumia lugha wasiyoelewa, tunawafundisha wanafunzi wetu kushindwa! Wengi wao wanajifunza kutodadisi, kutofikiri, kutokuuliza maswali, kunakili na kukariri, kuwa waoga, kutojiamini, kukubali kila hali na kukata tamaa kwa kauli ya “yote maisha”. Ni vyema tukajiuliza, kuandaa vijana wasioweza kuelewa, kujadili, kufikiri, kuchambua na kuchanganua masuala na dhana mbalimbali zinazofundishwa ni kwa masilahi ya nani? Ni wazi kwamba tunahitaji elimu ya kujikomboa na kwamba ili kufanikisha elimu ya kujikomboa shuleni na vyuoni, ni lazima wanafunzi watumie lugha ambayo wao na walimu wao wana uelewa wa hali ya juu.
Katika hali ambayo wanafunzi wana uelewa mdogo wa lugha, wanafunzi wengi, hasa wasichana, huwa wanyonge na kwa muda mwingi hunakili maandiko ya mwalimu (mengine yakiwa na makosa) kwa kadri watakavyoweza kuyasoma. Maandiko hayo kwa sehemu kubwa wengi hawayaelewi.
Badala ya kujifunza masuala ya msingi, wanafunzi wanaishia kukariri maneno kwa lugha wasiyoelewa na muda mwingi unapotea na ari ya kusoma inapungua. Elimu hii ya kunakili na kukariri haiwapi uwezo wa kujikomboa bali huenda kinyume na makusudio.Kama tunataka maendeleo ya kweli, Waafrika ni lazima wachukue mamlaka juu ya taratibu zinazotumika kuendesha elimu yao. Lazima wafundishe watoto wao kwa lugha wanazoelewa ili kuwaandaa kuwa wadadisi wa kutafuta majibu ya matatizo yanayoikabili jamii. Ikumbukwe kuwa lengo kuu la elimu ni maendeleo siyo umahiri wa lugha fulani. Ni falsafa mbadala!

Jumapili, 6 Julai 2014

umuhimu wa Kiswahili kama Lugha ya kufundishia elimu ya sekondari


Lugha ya kufundishia Sekondari ni Kiingereza. Wadau wengi wanasema hii ni sababu moja ya vijana kutoelewa/kufeli. Tufundishe kwa Kiswahili? Sote tunatambua kwamba Elimu ndio nguzo muhimu kwa maendeleo na katika kurekebisha Elimu yetu suala la lugha ni muhimu. Tutafakari pia msingi wa elimu ni nini hasa? Msingi wa elimu ni kupata maarifa na kuyatumia kujiendeleza na kujenga jamii. Sababu ya elimu ni kupata maendeleo. Elimu sio kwa ajili ya ajira tu. Shabaha ya elimu pia ni kujenga udadisi na ubunifu katika kutafuta majawabu ya changamoto ndani ya jamii. Je maarifa hayawezi kupenyezwa kwa Kiswahili? Tukisema Kiswahili hakijitoshelezi maana yake tunakatia tamaa uwezekano wa kukipanua? Katika nchi ndogo lakini zilizoendelea - Sweden, Norway, Denmark, Finland - lugha zilizotumika kuvumbua mambo ni zao. Hii haiwezekani hapa kwetu? Je ni kweli watu hufikiria kwa lugha yake ya asili? Ukimlazimisha mtu afikirie, abaini na avumbue kwa lugha isiyo yake ataweza au ataiga tu? Lugha sio kwa ajili ya mawasiliano tu na walimwengu wengine. Lugha pia ni kwa ajili ya kujenga fikra na kujitambua. Elimu haina majibu ya shida zote za jamii. Na elimu ya kukaririsha majibu haifai. Elimu inapaswa kujenga uwezo na maarifa ya kutafuta MAJAWABU.

na january makamba

Jumanne, 1 Julai 2014

nini kinaendelea kwenye shule zetu?

Mwananchi 1 tu kati ya 10 ndiye anayefikiri kuwa watoto wengi wanaomaliza darasa la 2 wana uwezo wa kusoma na kufanya hisabati wa darasa hilo hilo (ngazi ya darasa la 2). Mbaya zaidi, wananchi 3 tu kati ya 10 (31%) wanafikiri kuwa watoto hawa wanapaswa kuwa na uwezo wa kusoma na kuhesabu kwenye ngazi yao; ikimaanisha kuwa wananchi hawana matumaini kama kweli mfumo wa elimu utawafundisha watoto ujuzi na stadi wanazotakiwa kupata wakiwa shuleni.
Matokeo haya yalitolewa na Twaweza kwenye muhtasari wa utafiti wenye jina la Nini kinaendelea kwenye shule zetu? Wananchi watafakari juu ya hali ya elimu. Muhtasari huu umetokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza Afrika kwa njia ya simu mkononi wenye uwakilishi wa kitaifa ambao unauwakilishi wa kaya zote Tanzania Bara.
Muhtasari huu unachunguza hali ya shule zetu, ufundishaji na ujifunzaji pamoja na ushiriki wa wazazi kwenye elimu ya watoto wao. Licha ya matarajio ya chini kwenye mfumo wa elimu, wazazi mara nyingi hutimiza wajibu wao kuhamasisha na kusimamia ujifunzaji. Wanafunzi 7 kati ya 10 waliripoti kuwa wazazi wao hupitia na kukagua madaftari yao mara kwa mara.
Walimu wana wajibu wa kuhakikisha watoto wanajifunza shuleni. Hata hivyo, hawawezi kufanya kazi hii kama walimu wenyewe hawaingii darasani. Wanafunzi 3 kati ya 10 walithibitisha kuwa mwalimu wao muhimu aliingia darasani vipindi vyote siku iliyopita. Wanafunzi 4 kati ya 10 (38%) waliripoti kuwa mwalimu wao hakuingia darasani siku nzima, na wanafunzi 3 kati ya 10 (28%) walisema kuwa, mwalimu aliingia baadhi ya vipindi tu vya siku hiyo.
Sauti za Wananchi iliuliza pia maswali kuhusu hali ya mazingira ya shule. Karibu wanafunzi wote (99%) wanafundishwa wakiwa madarasani, siyo nje, na wanafunzi 9 kati ya 10 (91%) hukaa kwenye fomu au dawati shuleni. Hata hivyo, ni nusu tu ya idadi ya wanafunzi (49%) waliosema hupewa chakula shuleni. Ingawa kukosekana kwa viti na madarasa kuna uwezekano wa kuathiri viwango vya kujifunza, watoto wanapokuwa na njaa wanakuwa na uwezo mdogo kupokea na kumiliki maarifa mapya.

chanzo twaweza tanzania

Tatizo la mimba kwa wanafunzi wa kike, serikali bado kigugumizi

kassim majaliwa
Nilikuwa nikisikiliza maelezo ya Mbunge Kasim Majaliwa, akiwa Bungeni, kuhusiana na suala la mimba za utotoni, na kama ni vizuri wanafunzi wanaopata mimba wasirudishwe au warudishwe shuleni kuendelea na masomo baada ya kujifungua. Na kuwa kama  kurudishwa shule hakutakuwa ni mfano mbaya kwa wengine, au kutakuwa ni faida.

Mimi nataka kusema kuwa hakuna hasara yoyote kwa kumrudisha msichana shuleni baada ya kujifungua, na sababu ziko nyingi!
‘Kosa’ la mwanafunzi wa kike ni moja tu, kuwa na tumbo linaloweza kukaa mtoto, na kuonekana hadharani kuwa alijihusisha katika mapenzi na hakuweza kujikinga na hatimaye alipata mimba.

Na kuwa wale waliohusika (nasema ni wengi waliohusika) na kupatikana kwa mimba ya huyu msichana hawana tumbo kama hilo, au wamejitenga na uwajibikaji kwa kosa husika.

Kabla sijafika huko kwenye kutaja walio na makosa yaliyosababisha mimba, nataka niulize? Hivi kweli Tanzania, serikali na watu wake wako tayari kuendelea na maisha ya karne ya ishirini na moja wakiwa na watu wasiojua kusoma na kuandika, watu ambao wana elimu nusunusu, watu ambao hawana uwezo wa kuajiriwa na kujiajiri?

Kisa ni kuwa msichana huyu amepata mimba akiwa mtoto- tena mimba ya utoto! Msichana huyu atakuwa ni mzigo kama asipoachwa aendelee na masomo, na hataweza kumudu maisha yake.

Katika nchi ambayo inataka kila mtu awe mjasiriamali, haiwezi kuruhusu kikundi cha watu wachache au wengi kuishi bila elimu, au elimu ya kutosha. Msichana huyu ataturudishwa nyuma kimaendeleo kama akiachwa asiendelee na shule kwa kosa dogo la mimba.

Waliohusika na kupatikana kwa mimba kwa huyu mtoto ni wazazi? Wazazi wajiulize kama walikaa na mtoto ambaye tayari amekua na kubalekhe, ili kumpa mwongozo bora wa maisha na umuhimu wa elimu kwake, na umuhimu wa urafiki na watu wa rika mbalimbali, lakini wakiwa waangalifu kuhusiana na suala la mapenzi? Au wazazi walitegea walimu, na walimu hawakuwajibika ipasavyo kwani walidhani kuwa wajibu wao ni kuwapatia elimu tu, ambayo ni masomo ya msingi bila kuhusisha stadi za mahusiano na maisha? Walimu wamekuwa wakiwalea watoto kwa muda wa kati ya saa 6 kwa siku hadi saa kumi na mbili, na wakati mwingine kwa miezi mitano hadi kumi kwa mwaka.

Hawa ni wazazi wa pili wa mwanafunzi huyu mdogo kwa umri, asiye na stadi kamilifu za mahusiano, na hawampatii mafunzo kuhusiana na hilo. Ukienda shule nyingi hakuna mfumo wa elimu ya unasihi ambapo mtoto anaweza kufika ofisini kwa mnasihi akihisi anasumbuliwa na mahusiano, au anataka kujiingiza kwenye mahusiano lakini hana uhakika na njia sahihi ya kuenda nayo.

Mtoto anajikuta akiishi kwa kubahatisha katika mahusiano ambao mengi yanaainisha ngono kama ndiyo msingi wa mahusiano. Na utaona hao hili lilimsababishia mtoto kupata mimba, ingawa eti lawama zinabaki kwa mtoto.

Watoto wanapotoka kwenye familia ya masikini, na kufika katika jamii ambako watoto wenzao wanakula vyakula vizuri, wana mali za kisasa, na wanaishi wakiwa na fedha zao wenyewe walizopewa na wazazi, siyo rahisi kujitoa katika mitego kama miongo ya kimalezi ya wazazi na ya shuleni ni hafifu au haipo.

Watoto hawa wanzongwa na mifumo ya habari na tamaduni pendwa ambavyo  vinawachagiza kujiingiza katika mahusiano au tabia ambazo zitawaingiza katika mahusiano bila kuwa na mwongozo sahihi.

Na watoto kama wageni katika dunia hii, wanapaswa kuwasaidia kuwaongoza watoto hao ili waelewe maana ya vitu wanavyokutana navyo. Watoto wanatakiwa kuongozwa, na wengi wa watoto waliopata mimba utotoni hawakuongozwa vizuri. Hawa walihusika kumpatia mtoto mimba, kwa sababu hawakutimiza wajibu wao!

Kinanishangaza zaidi pale ambapo aliyehusika na kudunga mimba anajulikana, au hata kama hajulikani, anaachwa aendelee na maisha yake, na mtoto wa kike ndiye anayebeba lawama. Kwa hili hatutofautiani na wale ambao mwanamke na mwanaume wakikamatwa wanazini, anayepigwa mawe na kuuawa ni mwanamke; mwanamke akibakwa, anayepigwa mawe na kufa ni mwanamke.

Wakati mwanaume, aliyehusika kumbaka, tena inajulikana kuwa ndiye aliyefanya hivyo, anaachwa aishi kwa raha na starehe akiendelea kuvizia wanawake  wengine wa kubaka.

Angalia jinsi vyombo vya habari vinavyohusika na kuwaambia watoto kuwa mapenzi kati yao inawezekana. Michezo ya kuigiza ya televisheni, redio, magazeti, na filamu, vyote hivi vinawaambia wanaume na wanawake kuwa mapenzi ya watoto kwa watoto, watoto na watu wazima, yanawezekana.

Kwa kifupi utaona kuwa waliohusika na kupewa mimba msichana ni wengi kutokana na tabia zao, ulegevu wao katika malezi na sera, lakini eti msichana ndiye pekee anabakizwa na kosa.

Huu ni uonevu. Ndiyo maana ninashangaa kusikia serikali inasita kumtambua mtoto wa kike kuwa ni kiumbe asiye na kosa!