Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumatano, 26 Februari 2014

MATOKEO KIDATO CHA NNE 2013:Elimu yazikwa rasmi

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imetupiwa lawama kwa kuruhusu upangaji wa madaraja ya mitihani ya kidato cha nne unaozua utata na kuwa na dalili za kuzika elimu nchini.

Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule Binafsi  na Vyuo Visivyo vya Kiserikali (Tamongso), Benjamin Nkonya, ameiambia NIPASHE kuwa upangaji wa madaraja uliofanywa na Necta utaligharimu taifa kwa kiasi kikubwa kwani unaangamiza elimu badala ya kuiinua.

Nkonya alisema kuwa madaraja hayo mapya yaliyotumika katika kutangaza matokeo ya mtihani uliopita ya kidato cha nne yanaonekana kuwa na nia ya kuuonyesha umma kuwa watahiniwa wameanza kufanya vizuri zaidi na kujenga dhana kuwa kiwango cha elimu kinapanda kwavile imepanua wigo wa ufaulu bila kuzingatia haja ya kuboresha maeneo muhimu kama ya uandaaji wa mitaala sahihi na kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu yenyewe.

Alisema kuwa wao (Tamongso), walishapinga mara kadhaa utaratibu huo uliotumika sasa lakini wanashangaa kuona kuwa bado serikali kupitia Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) ikitumia madaraja yaleyale waliyokuwa wakiyapinga kila mara.

"Kwa mfano, sisi tulipendekeza alama za ufaulu zianzie angalau alama 35 hadi 50 kwa daraja la nne... wanaopata chini ya hapo watafutiwe utaratibu mwingine ikiwa ni pamoja na kuwapeleka kwenye vyuo vya ufundi. Lakini hilo halijazingatiwa na kilichopo sasa, ni siasa tupu katika elimu ambayo mwishowe itaua elimu," alisema Nkonya.

Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia, amesema matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa hivi karibuni ni danganya toto na kama siyo serikali kupandisha madaraja, yangekuwa mabaya kuliko ya mwaka jana kwani wengi waliofaulu, wakifuatilia kiundani ni sawa na wamefeli.

Alisema matokeo hayo ni kucheza na akili za Watanzania hususan walala hoi kwa kuwa katika shule za serikali ambazo kwa sasa zimegeuziwa kisogo, hakuna mtoto wa kiongozi au mtumishi wa umma mwenye kipato cha kati anayesoma huko.

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika ameitaka serikali kuboresha mazingira ya kutolea elimu ili kuinua kiwango na siyo kwa njia hii ya kubadili madaraja kwa namna inayotia shaka kwani huko ni kuangamiza elimu nchini.

"Serikali kwa barakoa (veil) ya kutekeleza Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now) imeamua kulificha taifa juu ya Matokeo Mabaya ya Sasa (Bad Results of Now).
Hivyo, wachambuzi wa masuala ya elimu wanapaswa kutoa takwimu za matokeo yangekuwa namna gani iwapo viwango vya awali vya ufaulu vingetumika ili nchi ijue hali halisi kwa manufaa ya wananchi," alisema Mnyika.

UTATA
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE kupitia matokeo yaliyotangazwa mwishoni mwa wiki umebaini kuwa mbali na wizara hiyo kushusha sana alama za ufaulu na hivyo kupunguza pia idadi ya watahiniwa waliofeli kutoka asilimia 56.92 ambayo ni sawa na wanafunzi 210,846 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 42.91 (wanafunzi 151,187), bado kumekuwa na matokeo yenye utata, hasa katika vigezo vya kuwapanga waliopata daraja sifuri na wale waliofaulu kwa kiwango cha walau daraja la nne.

Katika baadhi ya shule, NIPASHE imebaini kuwa matokeo hayo yamewachanganya watahiniwa kwa kiasi kikubwa, yakionyesha kuwa baadhi yao wamefeli kwa daraja sifuri licha ya kupata alama za jumla walizoamini kuwa zingewaweka katika kundi la waliofaulu kwa kiwango cha daraja la nne.

Aidha, wengine wamejikuta wakichanganywa pia na matokeo ya wenzao wanaoonekana kupata alama za jumla za chini zaidi lakini bado wakipewa daraja la nne.

Miongoni mwa matokeo hayo ya utata yanaonekana katika Shule ya Sekondari Wigamba iliyopo Mbeya mjini na pia katika Shule ya Sekondari Dr. Nchimbi, hasa tofauti ya alama kati ya madaraja ya nne na sifuri. Baadhi ya wanafunzi katika shule hizo wanaonekana kufeli vibaya kwa kupata daraja la sifuri, licha ya jumla ya alama walizopata kuonyesha kuwa ni 42.

Kwa mujibu wa upangaji mpya wa madaraja wa NECTA, daraja la sifuri huanzia alama 47 hadi 49 huku daraja la nne likiwa ni kwa ajili ya watahiniwa waliopata jumla ya alama zinazoanzia 32 hadi 46.

Katika shule ya Wigamba, mtahiniwa mvulana mwenye namba S3133/0054 anaonekana akiwa amepata daraja la sifuri licha ya kupata alama 43. Huyu amepata D ya English na E za masomo ya Civics, Kiswahili na Biology huku akiwa amefeli kwa kupata F katika masomo mawili ya Historia na Hisabati.

Hata hivyo, mtahiniwa mwingine katika shule hiyo hiyo ya Wigamba, mwenye namba S.3133/0010 amefaulu kwa kupata daraja la nne licha ya kwamba jumla ya alama zake kuwa 44, moja zaidi ya mtahiniwa S.3133/0054 aliyepata sifuri. Mwingine aliyepata sifuri licha ya kupata alama 42 ni mtahiniwa mwenye namba S.3133/0092 wakati mwenzake mwenye namba S.3133/0100 akifaulu kwa kiwango cha daraja la nne licha ya alama zake kuwa sawa na yeye ambazo ni 42.

Mifano mingine inayoashiria utata au kutoeleweka wazi kwa mfumo mpya wa madaraja ni pamoja na matokeo ya mtahiniwa mwenye namba S.1877/0007 wa Shule ya Sekondari ya Dr. Nchimbi. Huyu anaonekana kufaulu kwa kupata daraja la nne licha ya kuwa na pointi 46, akipata C ya Kiswahili na F za masomo sita ya Civics, History, Geography, English, Chemistry, Biology na Basic Maths.

Mtahiniwa mwenye namba S1877/0006 wa Shule ya Sekondari Dr. Nchimbi pia anaonekana kupata daraja la nne licha ya kuwa na alama 46 wakati mwanafunzi mwingine wa shule hiyo hiyo, mwenye namba S1877/0170 akifeli kwa kupata daraja sifuri licha ya kuwa na alama 46 kama mwenzake mwenye namba S1877/0006. 

Kwa mujibu wa NECTA, madaraja mapya yaliyotumika sasa yanaonyesha kuwa sawa na yale yaliyowahi kutangazwa na Profesa Sifuni Mchome na kupingwa na baadhi ya wabunge ambayo ni daraja la kwanza lililiobaki vilevile kuanzia alama za jumla 7 hadi 17, daraja la pili likibadilika kutoka 18-21 hadi 18-24, daraja la tatu kuwa 25-31 badala ya 22-25 ; daraja la nne kubadilika kutoka 26-32 na kuwa 32-46 huku daraja sifuri likiwa 47 hadi 49.

Aidha, katika utaratibu wa sasa, A huanzia 75-100; B+ ni 60-74; B ni 50-59 wakati C ni alama kuanzia 40 hadi 49. Mgawanyo mwingine unaonyesha kuwa D huhusisha alama kati ya 30 hadi 39, E ni 20 hadi 29 na F huhusisha ufaulu wa alama 0-19.

Hata hivyo, ilitarajiwa kuwa kutokana na mabadiliko hayo, wale waliopata alama za jumla kuanzia 32 hadi 46 wangekuwamo katika orodha ya waliofaulu kwa kiwango cha daraja la nne na siyo sifuri.  

NECTA YAFAFANUA
Akizungumzia kuhusu utata wa madaraja, Afisa Uhusiano wa Necta, John Nchimbi, aliiambia NIPASHE jana kuwa ufaulu wa daraja la nne hautegemei alama za jumla peke yake bali ni pamoja na sharti lake kuu ambalo ni lazima kila mtahiniwa awe amepata angalau D mbili na C moja.

Aliongeza kuwa kifungu cha 20 (6) cha Kanuni za Mitihani ndicho kinachoeleza wazi kuhusu vigezo vya ufaulu wa daraja la nne ambavyo ni pamoja na ulazima wa kufaulu kwa kiwango cha C au D mbili na siyo wingi wa alama.

Alieleza dhana nyingine za madaraja hayo mapya kuwa ni pamoja na kuangalia viwango vya ufaulu, kuanzia A hadi F ya makundi ya alama ambazo watahiniwa wamezipata; hilo likiambatana na mabadiliko yaliyopanua wigo kutoka makundi matano yaliyozoeleka awali (A, B, C, D NA F) hadi kufikia makundi saba ya A, B+, B, C, D, E na F.

Akitoa mfano, Nchimbi alisema kuwa mtahiniwa mwenye alama 42 anaweza kuwamo katika kundi la waliofeli kwa kupata daraja sifuri ikiwa atakosa sifa ya kuwa na walau C moja au D mbili.

Aidha, alieleza mazingira yanayoweza kumfanya mtahiniwa apate daraja la nne licha ya kuwa na jumla ya alama 46 kuwa ni pamoja na kupata C na kisha masomo sita kati ya saba yanayohesabiwa akawa amefeli yote kwa kupata F. 

Hata hivyo, haikufahamika mara moja kama wanafunzi wote waliofanya mtihani huo walishajulishwa juu ya upangaji huo mpya wa madaraja na kufanya mazoezi kupitia mitihani yao ya majaribio maarufu kama 'mock' na pia mitihani ya kawaida ambayo kidato cha nne huifanya wakati wote wanapojipima kwa maandalizi ya mtihani wa taifa.

BUNGE
Licha ya Necta kutoa ufafanuzi huo kuhusu madaraja, NIPASHE inatambua kuwa uamuzi wa baraza hilo umekiuka mapendekezo kadhaa ya wabunge wakati wakijadili kadhia ya matokeo mabaya ya mitihani ya kidato cha nne mwanzoni mwa mwaka 2012.

Katika majadiliano yao, wabunge wengi walipinga mapendekezo kadhaa ya kuwapo kwa madaraja mapya likiwamo la daraja la tano lililotangazwa awali mbele ya waandishi wa habari na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Mchome kabla serikali kumkana bungeni kupitia kauli iliyotolewa na aliyekuwa Naibu Waziri, Philip Mulugo, akisema kuwa hakuna daraja la tano na kwamba, daraja sifuri lililotangazwa kufutwa na Mchome linabaki palepale.

Matokeo yaliyotangazwa mwishoni mwa wiki na Kaimu Katibu wa Necta, Dk. Charles Msonde yalionyesha kuwa kwa ujumla, ufaulu umeongezeka kwa asilimia 15.17 kulinganisha na mwaka 2012, matokeo ambayo baadhi ya wadau wameyakosoa vikali.
 
chanzo ippmedia.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni