Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumamosi, 21 Septemba 2013

Chikombe: Shule yenye walimu watatu wanafunzi 300

Nikiwa ziarani mkoani Lindi nafanikiwa kupita katika shule mbalimbali za msingi na sekondari. Lengo hasa lilikuwa ni kuangalia mazingira halisi ya shule hizo kama yanaweza kuleta tija kwa siku za baadaye?

Shule ya msingi Chikombe ndiyo kambi yangu ya kwanza katika ziara hii. Kwa kutumia usafiri wa pikipiki nafanikiwa kufika shuleni hapa saa tano asubuhi, nikitokea Lindi Mjini.

Mbele yangu ni uwanja mkubwa wa nyasi ukiwa na miti michache ya miembe. Kuna wanafunzi wachache wakiwa wamezagaa katika eneo hilo wakicheza mpira. Hii inaashira kuwa wako kwenye muda wa mapumziko.

Kadiri ninavyosogea nazidi kuwa karibu na majengo ya shule mbele yangu. Ni majengo mawili yenye hali tofauti. Moja ni jengo lenye madarasa mawili na ofisi moja ndogo ya walimu linaloonekana kuwa jipya kidogo.

Pia jingine ni jengo kuukuu lililojengwa kwa udongo na miti. Kwa kulitazama jengo hili unaweza kulifananisha na zizi la ng’ombe ama stoo ya kuhifadhia vifaa vya kilimo. Jengo hili lina vyumba vitatu vinavyotumika kama madarasa.

Upana wa chumba kimoja cha jengo hilo unaweza kuwa ni urefu wa madawati mawili na uchochoro wa kupita mtu mmoja katikati.

Wanafunzi wa darasa la awali, la kwanza, la pili la tatu na la nne hutumia madarasa haya kama sehemu yao ya kusomea.

Kwa muda huu nilioingia nakuta wanafunzi wa darasa la kwanza wakiwa katika maandalizi ya kutoka shule.

Nafika kwenye ofisi ya walimu kwa ajili ya kujitambulisha na kupata mwenyeji wangu, ambaye ningepata mawili matatu kuhusiana na shule hiyo iliyo katika Wilaya ya Lindi Vijijini Jimbo la Mtama.

Mwalimu Hassan Halfan (54) ndiye alikuwa wa kwanza kukutana naye. Yeye ni mmoja kati ya walimu watatu katika shule hiyo. Kama ilivyo ada ya mgeni na mwenyeji alianza kwa kunipa historia ya shule yake.

“Shule ya Chikombe ilianza rasmi mwaka 2008 ikiwa na mwalimu mmoja ambaye ni mimi mwenyewe, nikiwa peke yangu niliweza kufundisha kwa miaka miwili bila usaidizi hadi mwishoni mwa mwaka 2009, alipokuja mwalimu mwenzangu,” alisema.

Mwaka 2010 idadi ya walimu iliongezeka na kufikia walimu watatu ambao tupo pamoja hadi hivi sasa.Changamoto kuu zinazoikabili shule hii

Kama ilivyo kwa shule nyingi zilizo katika Mkoa wa Lindi, Shule ya Chikombe inakabiliwa na matatizo lukuki kiasi cha kushindwa kujiendesha ipasavyo.Mradi pekee unaotegemewa katika shule hii ni ule wa shule ya awali, ambapo wazazi hulazimika kuwalipia watoto Sh300 kama ada ya mwanafunzi mmoja kwa mwezi.

“Pamoja na kuwekwa kwa kiasi kidogo cha ada, wazazi wanashindwa kuilipa na hivyo kuzidi kutupa wakati mgumu,” anasema mwalimu Halfani.

Anasema uchache wa walimu nalo ni tatizo linguine, ambapo walimu watatu waliopo wanalazimika kufundisha wastani wa vipindi 64 hadi 75 kwa wiki.
Jambo hili kwa kiasi kikubwa limekuwa likiwapa mtihani walimu hao na hata kushindwa kufanya shughuli zao kwa ufanisi.

“Uchache wa walimu umekuwa ukikwamisha maendeleo ya shule yetu kwa kiasi kikubwa sana. Lakini ukiachikia mbali uchache huo, hapa shuleni kwetu kuna uhaba wa nyumba za walimu,” anasema.

“Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, tulilazimika kuwaondoa wanafunzi katika darasa moja ili kumpisha mwalimu mkuu ambaye alikuwa hana nyumba ya kuishi,” anasema mwalimu Halfan.

Jambo hilo lilisababisha msongamano wa wanafunzi katika vyumba vya madarasa, kwani madarasa manne yalilazimika kutumiwa na mikondo saba na wengine ilibidi wafundishiwe nje ya madarasa anasema mwalimu huyo.

Baada ya kuona ukubwa wa tatizo hilo, wanakijiji waliingilia kati na kwa pamoja walishirikiana kujenga nyumba moja ya mwalimu mkuu, ili kuwapa wanafunzi nafasi ya kushiriki masomo darasani.
mwananchi.co.tz

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni