Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumanne, 1 Julai 2014

nini kinaendelea kwenye shule zetu?

Mwananchi 1 tu kati ya 10 ndiye anayefikiri kuwa watoto wengi wanaomaliza darasa la 2 wana uwezo wa kusoma na kufanya hisabati wa darasa hilo hilo (ngazi ya darasa la 2). Mbaya zaidi, wananchi 3 tu kati ya 10 (31%) wanafikiri kuwa watoto hawa wanapaswa kuwa na uwezo wa kusoma na kuhesabu kwenye ngazi yao; ikimaanisha kuwa wananchi hawana matumaini kama kweli mfumo wa elimu utawafundisha watoto ujuzi na stadi wanazotakiwa kupata wakiwa shuleni.
Matokeo haya yalitolewa na Twaweza kwenye muhtasari wa utafiti wenye jina la Nini kinaendelea kwenye shule zetu? Wananchi watafakari juu ya hali ya elimu. Muhtasari huu umetokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza Afrika kwa njia ya simu mkononi wenye uwakilishi wa kitaifa ambao unauwakilishi wa kaya zote Tanzania Bara.
Muhtasari huu unachunguza hali ya shule zetu, ufundishaji na ujifunzaji pamoja na ushiriki wa wazazi kwenye elimu ya watoto wao. Licha ya matarajio ya chini kwenye mfumo wa elimu, wazazi mara nyingi hutimiza wajibu wao kuhamasisha na kusimamia ujifunzaji. Wanafunzi 7 kati ya 10 waliripoti kuwa wazazi wao hupitia na kukagua madaftari yao mara kwa mara.
Walimu wana wajibu wa kuhakikisha watoto wanajifunza shuleni. Hata hivyo, hawawezi kufanya kazi hii kama walimu wenyewe hawaingii darasani. Wanafunzi 3 kati ya 10 walithibitisha kuwa mwalimu wao muhimu aliingia darasani vipindi vyote siku iliyopita. Wanafunzi 4 kati ya 10 (38%) waliripoti kuwa mwalimu wao hakuingia darasani siku nzima, na wanafunzi 3 kati ya 10 (28%) walisema kuwa, mwalimu aliingia baadhi ya vipindi tu vya siku hiyo.
Sauti za Wananchi iliuliza pia maswali kuhusu hali ya mazingira ya shule. Karibu wanafunzi wote (99%) wanafundishwa wakiwa madarasani, siyo nje, na wanafunzi 9 kati ya 10 (91%) hukaa kwenye fomu au dawati shuleni. Hata hivyo, ni nusu tu ya idadi ya wanafunzi (49%) waliosema hupewa chakula shuleni. Ingawa kukosekana kwa viti na madarasa kuna uwezekano wa kuathiri viwango vya kujifunza, watoto wanapokuwa na njaa wanakuwa na uwezo mdogo kupokea na kumiliki maarifa mapya.

chanzo twaweza tanzania

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni