
Serikali
inatafakari uwezekano wa kutanua wigo wa kutoa ruzuku hadi kwa shule
zinazomilikiwa na watu binafsi, ikiwa ni sehemu ya azma ya kuzipunguzia
gharama za uendeshaji.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George
Simbachawene, amesema hayo wakati akizungumza kwenye mahafali ya darasa
la saba katika Shule ya St. Anne Marie Academy jijini Dar es Salaam
jana.Alisema shule nyingi za binafsi zinafungwa kutokana na kushindwa
kujiendesha miongoni mwa sababu kubwa ikiwa ni kupanda kwa gharama za
uendeshaji.
Simbachawene alisema kuziacha shule binafsi `zife’
kutokana na sababu iliyo ndani ya uwezo wa nchi kuitatua, ni hasara kwa
taifa na kwamba njia pekee ya kuzisaidia kwa kuzipa ruzuku ili ziweze
kujiendesha.
Kwa mujibu wa Simbachawene, shule binafsi zimesaidia
kwa kiasi kikubwa kuinua kiwango cha elimu, hivyo kupunguza idadi na
kasi ya Watanzania kupeleka watoto wao kusoma nje ya nchi.Alisema:
"Ukiacha shule kama hii (St. Anne Marie) ikafa ni hasara kwa taifa,
serikali inaangalia kuona namna bora ya kuzisaidia kwa kuzipatia ruzuku
ili kuzipunguzia gharama za uendeshaji.”
Kwa upande mwingine,
Simbachawene aliwaasa vijana kuwa makini katika kukabiliana na
kuzishinda changamoto zilizo katika jamii, ikiwamo maambukizi ya Virusi
vya Ukimwi (VVU) na matumizi ama usafirishaji wa dawa za kulevya.
Meneja
wa shule hiyo, Jasson Rweikiza, alisema serikali imekuwa na kigugumizi
katika mambo mbalimbali katika sekta ya elimu, hali inayosababisha
kudumaa kwa sekta hiyo na watoto kukosa ufaulu mzuri.
Kwa mujibu
wa Rweikiza ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba Vijijini, mpaka sasa mitaala
ya elimu na sera za elimu hazipo wazi, hali inayosababisha walimu wakose
mwongozo wa kufundishia.
Alisema wadau wa elimu hususani
wamiliki wa shule binafsi, wanakabiliwa na kazi kubwa ya uendeshaji,
huku kukiwa na changamoto kadhaa kama vile matumizi ya mitaala
isiyoeleweka.
Pia alisema sera zinazohusiana na elimu hazipo
wazi, na kutoa mfano kuwa sera haielezi kama ni kosa ama si kosa
inapotokea kuwapo mwanafunzi asiyejua kusoma.
“Maendeleo hayawezi
kwenda bila kuboresha sekta ya elimu...tunaiomba serikali isimame imara
katika kuinusuru sekta ya elimu nchini,” alisema.
Rweikiza
alisema wahitimu wa darasa la saba wanapaswa kuondokana na dhana
inayowafanya kujiona wamemaliza shule, bali kiwango hicho kuwa msingi wa
safari ndefu inayowakabili maishani.
ippmedia.com