Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumapili, 6 Julai 2014

umuhimu wa Kiswahili kama Lugha ya kufundishia elimu ya sekondari


Lugha ya kufundishia Sekondari ni Kiingereza. Wadau wengi wanasema hii ni sababu moja ya vijana kutoelewa/kufeli. Tufundishe kwa Kiswahili? Sote tunatambua kwamba Elimu ndio nguzo muhimu kwa maendeleo na katika kurekebisha Elimu yetu suala la lugha ni muhimu. Tutafakari pia msingi wa elimu ni nini hasa? Msingi wa elimu ni kupata maarifa na kuyatumia kujiendeleza na kujenga jamii. Sababu ya elimu ni kupata maendeleo. Elimu sio kwa ajili ya ajira tu. Shabaha ya elimu pia ni kujenga udadisi na ubunifu katika kutafuta majawabu ya changamoto ndani ya jamii. Je maarifa hayawezi kupenyezwa kwa Kiswahili? Tukisema Kiswahili hakijitoshelezi maana yake tunakatia tamaa uwezekano wa kukipanua? Katika nchi ndogo lakini zilizoendelea - Sweden, Norway, Denmark, Finland - lugha zilizotumika kuvumbua mambo ni zao. Hii haiwezekani hapa kwetu? Je ni kweli watu hufikiria kwa lugha yake ya asili? Ukimlazimisha mtu afikirie, abaini na avumbue kwa lugha isiyo yake ataweza au ataiga tu? Lugha sio kwa ajili ya mawasiliano tu na walimwengu wengine. Lugha pia ni kwa ajili ya kujenga fikra na kujitambua. Elimu haina majibu ya shida zote za jamii. Na elimu ya kukaririsha majibu haifai. Elimu inapaswa kujenga uwezo na maarifa ya kutafuta MAJAWABU.

na january makamba

Jumanne, 1 Julai 2014

nini kinaendelea kwenye shule zetu?

Mwananchi 1 tu kati ya 10 ndiye anayefikiri kuwa watoto wengi wanaomaliza darasa la 2 wana uwezo wa kusoma na kufanya hisabati wa darasa hilo hilo (ngazi ya darasa la 2). Mbaya zaidi, wananchi 3 tu kati ya 10 (31%) wanafikiri kuwa watoto hawa wanapaswa kuwa na uwezo wa kusoma na kuhesabu kwenye ngazi yao; ikimaanisha kuwa wananchi hawana matumaini kama kweli mfumo wa elimu utawafundisha watoto ujuzi na stadi wanazotakiwa kupata wakiwa shuleni.
Matokeo haya yalitolewa na Twaweza kwenye muhtasari wa utafiti wenye jina la Nini kinaendelea kwenye shule zetu? Wananchi watafakari juu ya hali ya elimu. Muhtasari huu umetokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza Afrika kwa njia ya simu mkononi wenye uwakilishi wa kitaifa ambao unauwakilishi wa kaya zote Tanzania Bara.
Muhtasari huu unachunguza hali ya shule zetu, ufundishaji na ujifunzaji pamoja na ushiriki wa wazazi kwenye elimu ya watoto wao. Licha ya matarajio ya chini kwenye mfumo wa elimu, wazazi mara nyingi hutimiza wajibu wao kuhamasisha na kusimamia ujifunzaji. Wanafunzi 7 kati ya 10 waliripoti kuwa wazazi wao hupitia na kukagua madaftari yao mara kwa mara.
Walimu wana wajibu wa kuhakikisha watoto wanajifunza shuleni. Hata hivyo, hawawezi kufanya kazi hii kama walimu wenyewe hawaingii darasani. Wanafunzi 3 kati ya 10 walithibitisha kuwa mwalimu wao muhimu aliingia darasani vipindi vyote siku iliyopita. Wanafunzi 4 kati ya 10 (38%) waliripoti kuwa mwalimu wao hakuingia darasani siku nzima, na wanafunzi 3 kati ya 10 (28%) walisema kuwa, mwalimu aliingia baadhi ya vipindi tu vya siku hiyo.
Sauti za Wananchi iliuliza pia maswali kuhusu hali ya mazingira ya shule. Karibu wanafunzi wote (99%) wanafundishwa wakiwa madarasani, siyo nje, na wanafunzi 9 kati ya 10 (91%) hukaa kwenye fomu au dawati shuleni. Hata hivyo, ni nusu tu ya idadi ya wanafunzi (49%) waliosema hupewa chakula shuleni. Ingawa kukosekana kwa viti na madarasa kuna uwezekano wa kuathiri viwango vya kujifunza, watoto wanapokuwa na njaa wanakuwa na uwezo mdogo kupokea na kumiliki maarifa mapya.

chanzo twaweza tanzania

Tatizo la mimba kwa wanafunzi wa kike, serikali bado kigugumizi

kassim majaliwa
Nilikuwa nikisikiliza maelezo ya Mbunge Kasim Majaliwa, akiwa Bungeni, kuhusiana na suala la mimba za utotoni, na kama ni vizuri wanafunzi wanaopata mimba wasirudishwe au warudishwe shuleni kuendelea na masomo baada ya kujifungua. Na kuwa kama  kurudishwa shule hakutakuwa ni mfano mbaya kwa wengine, au kutakuwa ni faida.

Mimi nataka kusema kuwa hakuna hasara yoyote kwa kumrudisha msichana shuleni baada ya kujifungua, na sababu ziko nyingi!
‘Kosa’ la mwanafunzi wa kike ni moja tu, kuwa na tumbo linaloweza kukaa mtoto, na kuonekana hadharani kuwa alijihusisha katika mapenzi na hakuweza kujikinga na hatimaye alipata mimba.

Na kuwa wale waliohusika (nasema ni wengi waliohusika) na kupatikana kwa mimba ya huyu msichana hawana tumbo kama hilo, au wamejitenga na uwajibikaji kwa kosa husika.

Kabla sijafika huko kwenye kutaja walio na makosa yaliyosababisha mimba, nataka niulize? Hivi kweli Tanzania, serikali na watu wake wako tayari kuendelea na maisha ya karne ya ishirini na moja wakiwa na watu wasiojua kusoma na kuandika, watu ambao wana elimu nusunusu, watu ambao hawana uwezo wa kuajiriwa na kujiajiri?

Kisa ni kuwa msichana huyu amepata mimba akiwa mtoto- tena mimba ya utoto! Msichana huyu atakuwa ni mzigo kama asipoachwa aendelee na masomo, na hataweza kumudu maisha yake.

Katika nchi ambayo inataka kila mtu awe mjasiriamali, haiwezi kuruhusu kikundi cha watu wachache au wengi kuishi bila elimu, au elimu ya kutosha. Msichana huyu ataturudishwa nyuma kimaendeleo kama akiachwa asiendelee na shule kwa kosa dogo la mimba.

Waliohusika na kupatikana kwa mimba kwa huyu mtoto ni wazazi? Wazazi wajiulize kama walikaa na mtoto ambaye tayari amekua na kubalekhe, ili kumpa mwongozo bora wa maisha na umuhimu wa elimu kwake, na umuhimu wa urafiki na watu wa rika mbalimbali, lakini wakiwa waangalifu kuhusiana na suala la mapenzi? Au wazazi walitegea walimu, na walimu hawakuwajibika ipasavyo kwani walidhani kuwa wajibu wao ni kuwapatia elimu tu, ambayo ni masomo ya msingi bila kuhusisha stadi za mahusiano na maisha? Walimu wamekuwa wakiwalea watoto kwa muda wa kati ya saa 6 kwa siku hadi saa kumi na mbili, na wakati mwingine kwa miezi mitano hadi kumi kwa mwaka.

Hawa ni wazazi wa pili wa mwanafunzi huyu mdogo kwa umri, asiye na stadi kamilifu za mahusiano, na hawampatii mafunzo kuhusiana na hilo. Ukienda shule nyingi hakuna mfumo wa elimu ya unasihi ambapo mtoto anaweza kufika ofisini kwa mnasihi akihisi anasumbuliwa na mahusiano, au anataka kujiingiza kwenye mahusiano lakini hana uhakika na njia sahihi ya kuenda nayo.

Mtoto anajikuta akiishi kwa kubahatisha katika mahusiano ambao mengi yanaainisha ngono kama ndiyo msingi wa mahusiano. Na utaona hao hili lilimsababishia mtoto kupata mimba, ingawa eti lawama zinabaki kwa mtoto.

Watoto wanapotoka kwenye familia ya masikini, na kufika katika jamii ambako watoto wenzao wanakula vyakula vizuri, wana mali za kisasa, na wanaishi wakiwa na fedha zao wenyewe walizopewa na wazazi, siyo rahisi kujitoa katika mitego kama miongo ya kimalezi ya wazazi na ya shuleni ni hafifu au haipo.

Watoto hawa wanzongwa na mifumo ya habari na tamaduni pendwa ambavyo  vinawachagiza kujiingiza katika mahusiano au tabia ambazo zitawaingiza katika mahusiano bila kuwa na mwongozo sahihi.

Na watoto kama wageni katika dunia hii, wanapaswa kuwasaidia kuwaongoza watoto hao ili waelewe maana ya vitu wanavyokutana navyo. Watoto wanatakiwa kuongozwa, na wengi wa watoto waliopata mimba utotoni hawakuongozwa vizuri. Hawa walihusika kumpatia mtoto mimba, kwa sababu hawakutimiza wajibu wao!

Kinanishangaza zaidi pale ambapo aliyehusika na kudunga mimba anajulikana, au hata kama hajulikani, anaachwa aendelee na maisha yake, na mtoto wa kike ndiye anayebeba lawama. Kwa hili hatutofautiani na wale ambao mwanamke na mwanaume wakikamatwa wanazini, anayepigwa mawe na kuuawa ni mwanamke; mwanamke akibakwa, anayepigwa mawe na kufa ni mwanamke.

Wakati mwanaume, aliyehusika kumbaka, tena inajulikana kuwa ndiye aliyefanya hivyo, anaachwa aishi kwa raha na starehe akiendelea kuvizia wanawake  wengine wa kubaka.

Angalia jinsi vyombo vya habari vinavyohusika na kuwaambia watoto kuwa mapenzi kati yao inawezekana. Michezo ya kuigiza ya televisheni, redio, magazeti, na filamu, vyote hivi vinawaambia wanaume na wanawake kuwa mapenzi ya watoto kwa watoto, watoto na watu wazima, yanawezekana.

Kwa kifupi utaona kuwa waliohusika na kupewa mimba msichana ni wengi kutokana na tabia zao, ulegevu wao katika malezi na sera, lakini eti msichana ndiye pekee anabakizwa na kosa.

Huu ni uonevu. Ndiyo maana ninashangaa kusikia serikali inasita kumtambua mtoto wa kike kuwa ni kiumbe asiye na kosa!

Jumanne, 17 Juni 2014

Hali ya Elimu Tanzania

moja ya darasa shule ya msingi Bisumwa wilaya ya butiama


nchi haiwezi kuendelea na watu wachache wanaopata fursa za kipekee kwenye shule chache huku elimu ya jamii pana ikiwa mashakani. Hakuna haja ya kulumbana wala kuingiza siasa katika elimu, bali serikali itekeleze mipango na sera zilizopo na kuboresha mapungufu kwa kushirikisha wadau, na ukweli wa hali ya elimu nchini usisulubiwe wala kubezwa bali tuupokee na kuuwekea mikakati kwa pamoja tuweze kuboresha elimu yetu. pa kuanzia ni kila mmoja katika eneo lake,na kikubwa kufanya zaidi ya mazoea

Jumatano, 11 Juni 2014

changamoto ya elimu toka Geita


Walimu 97 katika shule ya msingi Nyankumbu na Mkombozi katika Wilaya ya Geita, wanatumia tundu moja la choo ambacho kipo kwenye nyumba ya mwalimu huku wanafunzi wa shule hizo 3,563 wakitumia matundu 14 ya choo na kuhofiwa kutokea magonjwa ya milipuko.

chanzo. jamii forums

Jumanne, 10 Juni 2014

kelele za Mbatia kuhusu ubora wa elimu je anasikilizwa?

james mbatia
Mbunge James Mbatia unajisumbua. Natambua uchungu ulio nao juu ya kudorora kwa sekta ya elimu, na natambua uhitaji wako wa mabadiliko katika sekta hii mapema inavyowezekana, lakini unajisumbua.

Sisemi kuwa ukate tamaa, na mimi sikati tamaa, ila naona unazungumza na watu ambao hawawezi kuelewa maana ya kile unachosema na kuhimiza. Nataka nieleza yafuatayo.

Mwaka jana ulipozungumza kuhusu mitaala, kuwa hakuna na kuwa sekta ya elimu inaendeshwa mzobemzobe kama Waluguru ambavyo wangesema, na kuwa vitabu vinavyotumika katika shule zetu havina uhakika wa ubora wake walikubeza, walikutukana, walikutenga, na kukuona mzushi.

Lakini wiki mbili baada ya kuahirishwa kwa Bunge, matokeo ya mitihani yakatoka, na kilichotokea, kuhusu kufeli kwa wanafunzi, Mungu tu anajua.
Mungu alikulipia na kuwaaibisha wale waliodhani kuwa ulikuwa mzushi, na ukarabati uliofanyika kuhusiana na matokeo hayo, na unaondelea kufanyika, sijui, ni suala la kuliombea taifa liondokane na pepo huyu ambaye hataki sisi tulioko serikalini tusikilize mawazo ya wananchi wenzetu.

Kuwa wananchi wenzetu wanapotushauri wanaonekana kuwa ni adui, na kuwa lengo lao sio kujenga ufanisi katika kutoa huduma bali kwa waliotupigia kura, bali kwa sababu wanataka kutujengea hoja tushidwe uchaguzi ujao.

Mbatia, unapokuwa na serikali ambayo wasiwasi wake ni kama itashindwa uchaguzi wa miaka mitano ijayo, na sio kama miaka mitano ijayo watakuwa na cha kuwaonyesha wananchi, katika orodha ndefu ya ahadi ndani na nje ya ilani ya uchaguzi waliyoinadi, sidhani kama unachokisema kitaeleweka.

Tumeona mwaka 2011, mara baada ya uchaguzi malumbano yakaanza ndani ya wanaserikali na walioko nje ya serikali, lakini wote wa chama kimoja, wakifanya maandalizi ya uchaguzi wa 2015.

Vikundi vya uchaguzi wa 2010 havikuvunjwa, kwa kweli vikaimarishwa na kampeni za uchaguzi kiaina zikaanza kwa makini kabisa, hadi walipoonyana wenyewe kwa wenyewe, lakini wale wenye masikio magumu wanaendelea bila kujali kitu.

Sasa hawa watu unapowaambia kuhusu kuimarisha sekta ya elimu unadhani inawezekana kweli, mawazo sio katika huduma bali katika kufanikisha chaguzi.

Mbunge Mbatia, maendeleo kwa wananchi kwa sasa, wewe unajua, sio kigezo cha kuchaguliwa. Hizo siasa zako ni za kizamani.

Sasa hivi unachaguliwa kwa sababu unaweza kutoa takrima, unaweza kuwanunulia watu ubwabwa wakashiba, ukawanunulia watu t-shirts, kofia na khanga, na kuwaimbisha nyimbo jioni wakala wakashiba.

Wananchi wa siku hizi hawaoni uhakiki wa utendaji wa walio madarakani kama ni kigezo, bali uwezo wake wa kutoa rushwa kwa wapiga kura. Sasa unapokuwa na uhakika wa kushinda kwa kutumia fedha na sio utendaji, unaanzaje kufikiria kuboresha elimu.

Elimu haikuwa kwenye ajenda wakati wa uchaguzi, ilitamkwa majukwaani kwa sababu mdomo haukosi cha kuzungumza ukikaa mbele ya kinasa sauti.

Kitu kingine ambacho unanishangaza James Mbatia ni kuwa huoni dunia inakwendaje?. Fasheni siku hizi ni kuhakikisha kuwa  watoto wanakwenda kusoma nje, na kama ni ndani basi katika shule za watu wakubwa, na wewe ukiwemo, nitashangaa kama haumo, kuwapeleka watoto kwenye English Medium, au sijui International Schools.

Unashangaa, mimi hapa ni waziri wa elimu, ofisa elimu, mkurugenzi wa elimu, mwalimu wa sekondari au mwalimu wa shule ya msingi, nimepewa dhamana ya kuhakikisha kuwa elimu inaboreshwa, na tulidhani kigezo kimojawapo ni kutuona sisi wenyewe tunawasomesha watoto wetu nje au ndani, lakini katika shule za serikali.

Lakini aka! Sasa kama tuliopewa dhamana ya kuboresha elimu tunakwepa shule zetu wenyewe, si ujue kuwa kuna jambo ambalo ni bovu tunaliona, na hatusemi ila tunawahamisha watoto wetu. Watoto wa masikini wajua wapi pa kuwapeleka wa kwao.

Kumeundwa kampeni kuwa wazazi wawagharimie watoto wao, badala ya kuimarisha shule za serikali, wanahimiza kuanzisha shule za binafsi.
Hivi kama kweli serikali ina nia ya kuboresha elimu, hao wazazi ambao wanalipa mabilioni ya fedha kwa ajili ya watoto wao, kama wangelipa robo tu ya hizo fedha kwenye shule za serikali kama ada, na serikali ikaweza kuboresha huduma na ubora wa, elimu, kungekuwa kweli na malalamiko dhidi ya sekta ya elimu?

Tungewaokoa wazazi wangapi ambao wanalipa ada kwenye shule ambazo hazina chochote ila utapeli. Lakini nadhani hatuwezi kufikiria kwa umakini.
Tunataka majibu rahisi kwa kitu kigumu, na hatutaki kufikiria kwa mkakati—strategically, bali kwa kuishi kama tulivyozoea.

Mbatia, tunahitaji kupungwa pepo huyu ambaye hataki kusikiliza vilio vya Watanzania kuhusu elimu.