Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Alhamisi, 6 Februari 2014

matatizo yanayomkumba mtoto wa kike kupata elimu bora

Kama kuna mikakati iliyobuniwa kuwasaidia watoto wa kike kupata elimu nchini, ni pamoja na ujenzi wa shule za sekondari za kata.
Pamoja na udhaifu wa shule hizo kama unavyojulikana kwa watu wengi, angalau sasa watoto wengi wa kike wanapata fursa ya kukaa shuleni kwa miaka minne badala ya kuozwa na kuwa mama katika umri mdogo na kuwa mwisho wa elimu yao.
Hata hivyo, mkakati huu pekee haujawa mwarobaini wa changamoto zinazowakabili watoto wa kike katika safari yao ya kuelekea kupata elimu. Bado kuna tatizo kubwa la umasikini uliokithiri na unaokuzwa zaidi na janga la Ukimwi katika jamii ya Kitanzania kiasi kwamba baadhi ya wasichana wanaoingia shule za sekondari hawaendelei muda mrefu.
Hawa wanalazimika kuacha shule ama mwanzoni au katikati kwa kukosa ada ama mahitaji mengine ya shule. Watoto wengi ni yatima na katika maeneo yaliyoathirika kwa kiwango kikubwa na tatizo la Ukimwi hata ndugu na jamaa wamelemewa na mzigo.
Tatizo hili nimeliona Mkoa wa Iringa na sehemu nyingine nchini. Kama utafiti ungefanyika kujua ukubwa wa tatizo hili ingekuwa ni jambo jema. Kwa hiyo, Serikali haina budi kubuni mikakati ya kuwapa fursa wasichana wa kutoka familia maskini na mayatima kumaliza elimu ya sekondari na vyuo vikuu.
Huko nyuma kumekuwepo mifuko ya misaada kama ule wa Shirika la Kimataifa la Misaada la Sweden (SIDA) na mingine, lakini kuna baadhi ya viongozi serikalini walipenyeza watoto wao na waliostahili wakakosa fursa hiyo. Hii ni tofauti na enzi za Mwalimu Julius Nyerere sisi tuliotoka familia maskini tuliweza kusoma hadi chuo kikuu bila matatizo. Cha msingi ni kuwa na sera nzuri inayoelekeza namna ya kuwapa fursa wasichana.
Umbali mrefu
Shule nyingi vijijini ziko mbali na makazi ya watu, hivyo wasichana wanalazimika kutembea masafa marefu kwenda na kurudi shuleni. Umbali huu una athari na hatari zake kwa watoto wa kike. Kwa mfano, wengi huchoka na mwishowe inawaathiri kimasomo.
Vilevile, katika safari hizo ndefu wasichana wengine huchokozwa na wahuni au hata kubakwa. Baadhi ya wazazi na walezi wamepangishia vyumba watoto wao karibu na shule. Suluhu hii imesababisha wasichana kuwekwa kinyumba na wanaume wakware na wasichana wengi wamepata ujauzito.
Tatizo hili la umbali pia huathiri hata walimu wa kike wanaopangwa kufundisha shule zilizo mbali vijijini ambako huduma za jamii kwa mfano usafiri, maji, umeme, nyumba na nyinginezo muhimu ni shida. Vilevile, walimu wa kike wanafanyiwa vitendo vya kihuni ama na walimu wenzao au hata wanajamii wengine vikiwamo vitendo vya kishirikina.
Mila za jamii ya wafugaji
Ingawa wilaya nyingi wasichana wako shuleni (msingi na sekondari) na hasa ukiangalia takwimu kitaifa, lakini wasichana kutoka jamii za wafugaji wengi wako majumbani kutokana na mila na desturi zao. Katika maeneo haya kuna shule chache na watoto hutembea masafa marefu kwenda shule na kurudi nyumbani.
Makabila haya ingawa yana utajiri wa mifugo, lakini ni wagumu kuiuza ili wasomeshe watoto wao hususan wa kike. Kwa sababu hii serikali inahitaji kubuni mkakati maalumu kutatua tatizo la usawa ili watoto wote wa kike kutoka makabila yote wapate elimu.
Katika nchi nyingi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini, ipo sera maarufu Kiingereza kwa jina la ‘Re-entry’.
Sera hii huruhusu wasichana wanaopata mimba wakiwa shuleni kuruhusiwa kuendelea na masomo hadi wanapojifungua na vilevile kuwaruhusu kurudi na kuendelea na masomo baada ya kujifungua.
Sera hii imejadiliwa na kupeleka pendekezo Wizara ya Elimu kwa muda mrefu, lakini haijulikani ni lini itapitishwa na kuwa sera au sehemu ya sheria ya elimu. Wasichana wengi kutoka familia maskini hupata ujauzito na kuacha elimu rasmi baada ya ujauzito.
Wale wanaotoka katika familia tajiri baada ya kujifungua hupelekwa shule binafsi na kuendelea na masomo. Hata hivyo, suala la ujauzito kwa wasichana ni kwa sababu tu ya maumbile yao.
Kama wavulana nao wangeumbwa kuweza kubeba mimba sielewi nani angebaki huko shuleni!
Viongozi wengi ngazi za kufanya uamuzi ni wanaume, hivyo hawaoni kwamba suala hili linahitaji lifanyiwe uamuzi upesi ili kuwanusuru wasichana wengi wanaoathirika badala ya kuwaona au kuwaita ni malaya.
Nipendekeze kwamba, kama suala hili la kuwa na mifuko ya elimu kwa ajili ya wasichana katika ngazi mbalimbali za masomo hususan shule za msingi na sekondari linakuwa zito kitaifa, litolewe mwongozo au sera ili litengewe fedha katika ngazi ya Halmashauri.
Ellen Binagi ni mdau na mwanaharakati wa masuala ya elimu.
Amewahi kufanya kazi katika mashirika na asasi mbalimbli zinazohusiana na elimu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni